John Mnyika
TANZIA: Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Chama Taifa, Mheshimiwa Regia Mtema ambaye pia ni Mbunge
wa Viti Maalum na Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira. Mheshimiwa Regia Mtema
amefariki leo tarehe 14 Januari 2011 kwa ajali ya gari katika eneo la
Ruvu darajani.
Katika uhai wake marehemu Regia ...Mtema
amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu
Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule
za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari
ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Machame. Marehemu
Regia Mtema alipata shahada yake ya kwanza (Bsc Home Economics and Human
Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine.
Mara
baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika
taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Afisa
Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa
kuwa Afisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi
ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti
maalum.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti
Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni,
Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa
chama makao makuu na wabunge wamejumuika hivi sasa na familia ya
marehemu katika kipindi hiki kigumu.
CHADEMA inatoa pole kwa
familia ya marehemu Regia Mtema, wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa
Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero kutokana na msiba huu wa ghafla
katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa chama na kwa taifa.
Taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya
kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mipango ya mazishi
ya marehemu inapangwa nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu
Estelatus Mtema, Tabata Chang'ombe. Ratiba ya maziko itatolewa baada ya
kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na familia ya marehemu, Ofisi ya
Bunge na chama.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.
Imetolewa na:
John Mnyika(Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment